Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
amewahimiza wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar kuunga mkono jitihada
zinazofanywa na serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
mapambano dhidi ya rushwa,ufisadi kama hatua ya kukomesha tabia hiyo
ambayo inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Makamu wa Rais Samia
Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo 13-Aug-16 wakati anahitimisha kilele cha
sikukuuu ya Wakizimkazi katika kijiji cha Kizimkazi Mkunguni wilayani
ya Kusini Unguja – Zanzibar ambaye yeye ni mwasisi wa sikukuu hiyo
ambayo inatumiwa na wakazi wa maeneo hayo kufanya michezo mbalimbali ya
jadi pamoja na kujadili na kuweka mipango na mikakati ya kujiletea
maendeleo kwa ushirikiano na viongozi wao.
Makamu wa Rais
amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa
watendaji wanaorudisha nyuma maendeleo ya wananchi ikiwemo ubadhirifu wa
fedha za umma ili kukomesha tabia hiyo.
Amesema kuwa ili wananchi
waweze kupata maendeleo ya haraka ni muhimu wananchi wakaimarisha
ushirikiano miongoni mwao katika kubaini changamoto zinazowakabili na
kushirikiane na viongozi wao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto
hizo.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema yeye kama kiongozi
wa kwanza kupata wadhifa huo kutoka kwenye kijiji cha Kizimkazi-
Zanzibar ataendelea kushirikiana wananchi hao kutatua matatizo
yanayowakabili wananchi hao ikiwemo tatizo la upatikanaji wa maji.
Makamu wa Rais pia amehimiza wananchi wa Kizimkazi kutafuta eneo haraka
kwa ajili ya ujenzi wa shule ya awali ambayo bado ni tatizo kubwa katika
eneo hilo ili aweza kuwasaidia katika ujenzi wake kama hatua ya kuondoa
kero ya watoto kushindwa kupata elimu ya awali.
Katika Risala
maalum ya wananchi wa kijiji cha Kizimkazi na Katibu wa Sherehe hizo
Said Ramadhani Mgeni kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Samia Suluhu Hassan wamewapongeza viongozi wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
jitihada wanazofanya za ukusanyaji wa mapato ya serikali na wamesema
wanaimani kubwa kuwa fedha zinazopatikana zitatumika katika kuinua
uchumi na kujenga ustawi wa Jamii bora wananchi.
Wananchi hao
wameahidi kuwa watadumisha na kuimarisha ushirikiano kati yao na
serikali hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Baadhi ya
Viongozi wa wilaya na Mkoa wa Kusini Unguja waliopata nafasi ya
kuzungumza katika hafla hiyo ya hutimisha sikukuu ya wakizimkazi
wamewaomba wananchi kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
13-Aug-16.
No comments:
Post a Comment